AU, IGAD na UN zaombwa kuingilia kati na kutatua mzozo kati ya Ethiopia na Somalia

Marion Bosire
2 Min Read

Baadhi ya wabunge wa eneo na kaskazini mashariki mwa Kenya sasa wanataka mashirika kama umoja wa Afrika AU, shirika la IGAD na umoja wa mataifa UN yaingilie kati na kutatua mzozo uliopo kati ya Ethiopia na Somalia.

Hii ni baada ya Ethiopia kuingia kwenye mapatano na eneo lililojitenga la Somaliland ambalo bado ni himaya ya Somalia bila kuzingatia uhuru wa taifa la Somalia.

Wabunge hao wakiongozwa na mbunge wa Dadaab Farah Maalim wanasema wamelazimika kupaaza sauti zao kutokana na uhusiano wa kiukoo uliopo kati ya watu wa kaskazini mashariki mwa Kenya na watu wa Somalia na uhusiano mwema wa kitaifa kati ya Kenya na Somalia.

Wanahisi kwamba iwapo suala hilo litasababisha vurugu basi huenda zikaathiri hata wakenya walio karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Ethiopia imekuwa ikitafuta namna ya kufikia bandari na badala ya kushirikiana na Somalia inayotambulika kimataifa ikaamua kuingia kwenye mapatano na Somaliland ambayo bado iko chini ya Somalia.

Mapatano hayo yanahusu Somaliland kuuzia Ethiopia eneo la kilomita 20 la bandari kwa miaka 50 huku Ethiopia ikiahidi kusaidia Somaliland ipate kutambulika kimataifa kama taifa huru.

Viongozi hao wanasema kwamba Ethiopia ambayo ni mwanachama wa umoja wa mataifa, umoja wa Afrika na ambayo ilitia saini mapatano kadhaa ya kimataifa ambayo yanathibiti mahusiano kati ya nchi huru imekosea kwa kufanya mambo visivyo.

Mashirika hayo matatu yanaombwa kuchukua hatua za haraka kufutilia mbali mapatano ya aina yoyote kati ya Somaliland na Ethiopia ili kuzuia vurugu.

Share This Article