Askofu mkuu wa kanisa la Kianglikana nchini, ACK Jackson Ole Sapit amelaani visa vya mauaji ya kutisha ya wanawake humu nchini.
Sapit anasema wakati umewadia wa visa hivyo vya mauaji kudhibitiwa kwani ni vya kinyama na kinyume cha mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
Anataka wahusika wa visa hivyo wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwa kuhatarisha maisha ya wasichana humu nchini.
Kulingana naye, visa hivyo vya wasichana wanaosaka pesa kwa kukubali kuhusika kwenye ngono vinazua maswali kuhusu usalama wa wanaotumia nyumba za kukodisha nchini hata kama ni muhimu kiuchumi.
Ushauri wa Sapit kwa wanafunzi ni kumakinika na masomo na kujiepusha na tabia ambazo zinaweza kudhuru maisha yao.
Matamshi ya Sapit yanafuatia kisa cha kuuawa kwa mwanafunzi wa chuo kikuu na mwili wake kupatikana huko Roysambu, Kasarani kaunti ya Nairobi.
Kisa kingine ni cha Starlet Wahu Mwangi ambaye alipatikana amefariki kwenye chumba cha kukodisha katika mtaa wa South B Nairobi.
Zipo ripoti pia za mwanamke kuuawa na mwili wake kurushwa kutoka kwenye nyumba yake ya kupangisha mtaani Lang’ata kaunti ya Nairobi.