Asasi za usalama zapokea shilingi bilioni 338 katika bajeti ya mwaka 2023/2024

Tom Mathinji
1 Min Read

Serikali imetengea asasi za usalama shilingi bilioni 338 katika bajeti ya mwaka 2023/2024, iliyowasilishwa bungeni siku ya Alhamisi na Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung’u.

Prof. Ndung’u alisema hatua hiyo iliafikiwa kutokana na jukumu muhimu linalotekelezwa la kuhakikisha mazingira salama hapa nchini.

Kati ya kitita hicho, shilingi bilioni 144.9, zimetengewa vikosi vya ulinzi (KDF), shilingi bilioni 98.6 zikatengewa huduma ya taifa ya polisi (NPS), shilingi bilioni 44.3 zikatengewa idara ya kitaifa ya Ujasusi (NIS) huku shilingi bilioni 31.3 zikitengewa idara ya magereza.

Aidha shilingi bilioni 8.8  zimetengwa kwa ukodeshaji ma magari za maafisa wa polisi huku shilingi bilioni 500 zikitumika kwa mipango ya kisasa, serikali inapojizatiti kuwapa maafisa wa polisi vifaa vya kisasa.

Na ili kuhakikisha vita dhidi ya uhalifu vinaimarishwa ili kufanikisha upatikanaji wa haki, Waziri huyo alisema shilingi milioni 856, zimetengwa ili kutoa vifaa vya kisasa kwa maabara ya kitaifa.

Prof. Ndung’u alisema bajeti hiyo pia imezingatia masilahi ya maafisa wa usalama huku akisema kuwa utawala wa Kenya kwanza utawapa makazi kupitia ushirikiano wa serikali na sekta ya kibinafsi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *