Asasi tatu kuu za serikali kuimarisha vita dhidi ya ufisadi

Tom Mathinji
2 Min Read

Asasi kuu tatu za Serikali zimekubali kufanya kazi pamoja kukabiliama na zimwi la ufisadi katika nyadhifa zao, Rais William Ruto amesema.

Serikali kuu, Bunge na Mahakama, alisema, zitatumia “mtazamo wa pamoja wa Serikali” kufikia lengo la kutokomeza uovu huo.

“Ninataka kuwaahidi watu wa Kenya kwamba tumeungana na tumeazimia kung’oa tatizo la ufisadi katika nchi yetu,” alisema.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi cha Gilgil Kaunti ya Nakuru, alisisitiza kuwa ufisadi, uzembe na masilahi ya kibinafsi yanadhoofisha maendeleo ya nchi.

Kiongozi wa nchi alitoa wito kwa viongozi wakiwemo viongozi wa mashirika ya kijamii, taasisi za kidini na upinzani kuja pamoja na kuunga mkono mapambano dhidi ya ufisadi.

Aliwataka walio katika upinzani kuacha kuingiza siasa katika mazungumzo kati ya tanzu hizo tatu za Serikali, na badala yake wachangie mawazo kuhusu jinsi mfumo wa sheria nchini na mahakama unavyoweza kuwezeshwa kukabiliana na ufisadi.

“Sio lazima kwetu kuwa na mabishano kuhusu jambo linalohitaji juhudi za pamoja za Wakenya wote,” alisema.

Rais Ruto aliwataka viongozi kuachana na siasa za ushindani na kuzingatia utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alisema itakuwa dharau kwa wananchi iwapo viongozi wataendelea kufanya siasa badala ya kuwasilisha ahadi walizotoa kwa Wakenya.

“Ninawaomba viongozi wote, haswa katika Kenya Kwanza, wawachane na mashindano kwa nafasi yoyote, ya sasa au ya baadaye, ili tuangazie kuwasilisha huduma kwa watu wa Kenya,” alisema.

Waliohudhuria ni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, Gavana wa Nakuru Susan Kihika na kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichungwa, miongoni mwa wengine.

TAGGED:
Share This Article