Mwanamuziki wa Nigeria Ahmed Ololade ambaye anafahamika na wengi kama Asake hatimaye ameridhia shinikizo za umma na kuchukua hatua za kuhudumia babake mzazi Fatai Odunsi.
Mzee Odunsi alikuwa ameomba usaidizi wa fedha za kugharamia matibabu yake kwani amekuwa akiugua kwa muda, suala lililowashangaza wengi ikitizamiwa kwamba mwanawe ni mwanamuziki mashuhuri ambaye ana pesa nyingi.
Mzee huyo alihojiwa na jamaa kwa jina Milgaga mitandaoni, ambapo alilalamika kwamba mwanawe Asake hakuwa amewasiliana naye kwa muda mrefu, akinyoshea mamake Asake kidole cha lawama kwa kutomsukuma mwanao amtafute.
Lakini Odunsi alifafanua kwamba hazozani naye tena kwani tayari amelipia matibabu yake na kwamba ametuma watu wamtafutie nyumba. Alisema pia kwamba ameahidi kutunza binti yake aliyemtelekeza pamoja na mama ya msichana huyo.
Nyumba inayotafutwa kulingana naye ni ambayo atanunuliwa na mwanawe hasa katika eneo la kisiwa jijini Lagos.
Katika mahojiano na Milgaga Odunsi alijitetea akisema alikuwa baba ambaye aliwajibika wakayi Asake alikuwa mdogo jambo ambalo pia lilithibitishwa na majirani wa mzee huyo.
Majirani hao katika eneo la Isale Eko, ambapo babake Asake anaishi wanasema kwamba mzee huyo aliwajibikia maslahi ya nyota huyo wa muziki wakati bado alikuwa mdogo.
Hadhi ya Asake kama mwanamuziki imekuwa ikipanda hasa baada yake kuteuliwa kuwania tuzo ya Grammy katika kitengo cha tumbuizo bora la muziki wa Afrika.