Siku 40 za mwizi zilitimia jana kwa familia ya baba na mwanawe wa kiume ambao wamekuwa wakiwaibia wafanyabiashara wa maduka ya Mpesa katika soko la Gikombaa, kaunti ya Nairobi.
Peter Mwendwa Musyoka aliye na umri wa miaka 49 na mwanawe mwenye umri wa miaka 23 Dennis Musyoka,walifumaniwa kwenye makazi yao mtaani Komarock, kufuaia msako ulioendeshwa na polisi wa ujasusi kutoka kituo cha Shauri Moyo.
Yamkini wawili hao walikuwa wameiba shilingi 236,000 kutoka kituo cha M-Pesa cha Gikomba Septemba 2.
Aidha, polisi walipata laini za simu mpya na nyingine ambazo zimetumika, vitambulisho vya kitaifa, nambari za wakala na nambari ya paybill kutoka kwa kampuni ya Safaricom na rununu zinazoaminika kuibwa.
Wawili hao wamewekwa rumande kusubiri kuwasilishwa kortini.