Kampuni ya Twiga Foods inanuia kupanua eneo la ardhi kwenye mradi wa Galana Kulalu wa uzalishaji vyakula kufikia ekari 20,000.
Upanuzi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mahindi kila mwaka hadi kufikia magunia milioni 2.
Mpango huo wa kampuni ya Twiga Foods, utatekelezwa kwa awamu mbili, baada ya kukamilishwa kwa ujenzi wa bwawa la Galana.
Mwanzilishi-mwenza wa kampuni hiyo ambaye pia ni mkurugenzi mkuu, Peter Njonjo, alisema upanuzi huo umejiri kufuatia miundo mbinu ya unyunyiziaji mashamba maji iliyowekwa.
“Kinyume na sehemu zingine za nchi, mahindi huchukua muda wa siku 105 kukomaa katika eneo hili. Hii inamaanisha kuwa kwa kutumia unyunyizaji maji mashamba, mahindi yatavunwa mara tatu kwa mwaka, tunalenga kuvuna magunia milioni mbili kwa mwaka,” alisema Njonjo.
Kufuatia agizo la Rais, bwawa la Galana linaendelea kujengwa na pendekezo la kuongeza Ekari elfu 350 zaidi, linaendelea kutathminiwa.
Kampuni ya Twiga Foods ionayoshirikiana na halmashauri ya kitaifa ya unyunyuziaji mashamba maji, tayari imeanzisha mpango wa majaribio wa zao la mahindi katika shamba la Ekari 538.