Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Samburu Moses Lenolkulal Kasaine amepatikana na hatia kwenye makosa kadhaa kwenye kesi ya ufisadi wa shilingi milioni 83 dhidi yake na washtakiwa wenzake 10.
Lenolkulal alipatikana na hatia ya kujipatia mali ya umma kinyume cha sheria na mahakama ya kupambana na ufisadi iliyoko Milimani jijini Nairobi.
Anatuhumiwa kwa mkinzano wa maslahi kufuatia hatua ya kutumia kampuni yake kwa jina “Oryx Service Station” kuwasilisha mafuta kwa serikali ya kaunti ya Samburu.
Mahakama iligundua kwamba kiongozi huyo wa zamani wa kaunti ya Samburu alitumia mtu mwingine kwa jina Hesbon Wachira, kutekeleza biashara hiyo. Wachira naye amepatikana na hatia ya kujipatia mali ya umma kinyume cha sheria.
Madai ya upande wa utetezi kwamba hakuna fedha zilizopotea wakati wa kutekeleza biashara hiyo yalikataliwa na mahakama.
Upande wa mashtaka ulikita kesi hiyo kwa ushahidi uliotolewa na mashahidi 11 na stakabadhi 388 vyote vikiashiria matumizi mabaya ya fedha za umma.
Lenolkulal na washtakiwa wenza, waligunduliwa kwamba walitumia mali ya umma kwa manufaa ya kibinafsi.
Hakimu mkuu Thomas Nzioki alisema kwamba ushahidi wa kutosha upo wa kuthibitisha kwamba Lenolkulal na wenzake wana hatia.