Serikali imezima matumaini ya wastawishaji wa ardhi wanaomiliki vipande viwili vya ardhi vinavyohusishwa na familia ya Kirima katika eneo la Njiru katika kaunti ya Nairobi.
Waziri wa Ardhi Alice Wahome amesema kuwa wako na rekodi zilizothibitishwa za ardhi na wanakubaliana na uamuzi wa mahakama kuwa ardhi hiyo ni ya mbunge wa zamani wa Starehe marehemu Gerishon Kirima.
Hii inatoa nafasi ya kufurushwa kwa watu wanaoishi kwenye ardhi hiyo kinyume cha sheria iwapo hawataafikiana na familia ya Kirima.
Wizara hiyo imewatahadharisha wale wanaoishi katika ardhi za umma karibu na vipande hivyo viwili vya ardhi huku ikisema kuwa vipande hivyo vitatwaliwa.
Haya yanajiri baada ya familia ya Kirima kujaribu kuwafurusha watu wanaoaminika kuishi katika ardhi ya familia hiyo katika eneo bunge la Kasarani kinyume cha sheria.
Agizo la mahakama lililotolewa Oktoba 23 mwaka huu liliwapa watu wanaoishi katika ardhi hiyo hadi Disemba 31 kuhama.
Hata hivyo, Rais William Ruto alipendekeza kuwepo kwa suluhu ya amani.
Waziri Wahome alisema serikali inalenga kutwaa ardhi zote za umma zilizonyakuliwa.