Alex Lemarkoko ndiye mhifadhi mkuu wa misitu humu nchini. Aliteuliwa kwa wadhifa huo kupitia mpango uliotekelezwa na bodi ya huduma ya kutunza misitu nchini Julai 31, 2023.
Lemarkoko ana tajriba katika uhifadhi wa misitu kwani alijiunga na iliyokuwa idara ya misitu nchini mwaka 1991.
Amehudumu kwenye nyadhifa mbalimbali kama vile naibu afisa wa misitu katika wilaya na baadaye akafanywa kuwa afisa wa misitu katika kiwango cha wilaya na amehudumu katika kaunti mbalimbali nchini.
Baadaye alihamishiwa makao makuu ya huduma ya kitaifa ya kulinda misitu ambapo alikuwa akishughulikia ulinzi wa misitu.
Lemarkoko amekuwa akihudumu kama kaimu mhifadhi mkuu wa misitu tangu mwezi Februari mwaka huu.
Ana shahada ya sayansi katika uhifadhi wa misitu kutoka Chuo Kikuu cha Moi na shahada ya Uzamili katika masuala ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Alifuzu pia kutoka taasisi ya ulinzi ya Kenya kando ka kozi fupifupi ambazo amesomea.
Lemarkoko ni mhusika mkuu pia katika kongamano la Afrika kuhusu biashara ya mbao na utunzaji misitu kati ya mataifa. Pia ni mwanachama wa chama cha wahifadhi misitu nchini Kenya.