Wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab wameshambulia hoteli moja kwa jina Syl, iliyo karibu na Ikulu ya Rais katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.
Hii ni kwa mujibu wa asasi za usalama nchini humo.
Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, milipuko na milio ya risasi ilisikika katika hoteli hiyo ambayo ni maarufu kwa maafisa a serikali.
“Mujahideen wenye silaha wanadhibiti hoteli hiyo na wanawapiga risasi wafanyakazi na maafisa wa serikali katika hoteli hiyo,” lilisema kundi la Al-Shabaab huku likidai kuhusika na shambulio hilo.
Kundi hilo limewahi kushambulia hoteli ya Syl ambayo ni maarufu kwa maafisa wa serikali.
Hata hivyo, haikuweza kubainika mara moja iwapo kulikuwa na majeruhi.
Mkazi Farah Ali, ambaye anaishi karibu na ofisi ya rais, aliiambia Reuters: “Kwanza tulisikia mlipuko mkubwa, na kisha milio ya risasi ikafuata. Tunafahamu kwamba wapiganaji wako ndani ya [hoteli] kwa sababu tunasikia wakifyatuliana risasi.”
“Wapiganaji kadhaa waliingia ndani ya jengo hilo kwa nguvu baada ya kuharibu ukuta wa pembezoni kwa mlipuko mkubwa,” afisa wa usalama aliambia AFP.
Hassan Nur, ambaye alitoroka kwa kupanda ukuta na kuruka upande wa pili, alisema: “Sijui kuhusu majeruhi lakini kulikuwa na watu wengi ndani wakati shambulio hilo lilipoanza.”
Mashuhuda wengine waliripoti kuona polisi wakiwasili ndani ya dakika chache baada ya shambulio hilo, ambalo lilisababisha makabiliano ya risasi na wanamgambo.
Mashambulizi yamepungua katika wiki za hivi karibuni huku usalama ukiimarishwa baada ya serikali kuzidisha mashambulizi yake ya kijeshi dhidi ya kundi hilo.
Al-Shabaab inadhibiti maeneo makubwa ya kusini na katikati mwa Somalia.