Akothee ajawa na furaha kwenye hafla ya ndoa ya binti yake

Prudence na mpenzi wake aitwaye Fairouz waliamua kusajili ndoa yao kwa serikali ya Ufaransa Jumamosi Machi 22, 2025

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Akothee alikuwa mwingi wa furaha pale ambapo alihudhuria hafla ya ndoa ya kiserikali ya binti yake wa tatu nchini Ufaransa.

Msichana huyo kwa jina Prudence na mpenzi wake aitwaye Fairouz waliamua kusajili ndoa yao kwa serikali Jumamosi Machi 22, 2025.

Akothee alichapisha kadi ya mwaliko aliyotumiwa na mkwewe huku akichambua maneno yaliyokuwemo ambapo Fairouz alimrejelea kama mama.

Prudence na Fairouz ambao walikuwa wanapendeza kwa mavazi yao ya kitenge walianza sherehe ya kuhalalisha ndoa yao katika jengo la serikali la Mairie de Rouen saa tatu asubuhi kabla ya kuandalia wageni wao chamcha katika hoteli ya Rodizio Brazil saa sita adhuhuri.

Mazungumzo katika hafla hiyo yalikuwa kwa lugha ya kiingereza na kifaransa.

Kupitia Facebook, Akothee alimsifia binti yake akitaja ndoa yake kuwa shahada ya tatu, “Tazama shahada rasmi ya tatu ambayo ni ndoto ya kila msichana. Binti yangu Fancy Makadia ametimiza tena. Shahada mbili na cheti kimoja cha ndoa.” aliandika.

Baadaye mama huyo wa watoto watano alifafanua kwamba alikwenda tu kushuhudia kutiwa saini kwa cheti cha ndoa na harusi yenyewe bado.

“Harusi ndio inakuja, hii hata sikuhitajika, ni babake tu atie saini kama shahidi kwamba amewabariki nimekuwa tu kaflower girl” aliandika Akothee akirejelea baba mlezi wa Prudence Dominique ambaye ni baba mzazi wa kitindamimba wa Akothee aitwaye Oyoo.

Mwanamuziki huyo ambaye pia ni mwanabiashara anasema anasubiri kwa hamu siku ambayo atapata fursa ya kumsindikiza binti yake kwenye harusi yake.

Website |  + posts
Share This Article