Ajali ya ndege iliyoua naibu rais wa Malawi yasemekana kusababishwa na hali mbaya ya hewa

Mwenyekiti wa tume iliyobuniwa kuchunguza ajali hiyo Jabbar Alide ndiye alisoma ripoti hiyo ambapo alielezea kwamba marubani wawili wa ndege hiyo walipoteza uwezo wa kuona kufuatia utandu wa mawingu na upepo mkali.

Marion Bosire
3 Min Read
Saulos Chilima

Ajali ya ndege iliyosababisha kifo cha naibu rais wa Malawi Saulos Chilima miezi sita iliyopita ilisababishwa na hali mbaya ya hewa na makosa ya kibinadamu, haya ni kulingana na ripoti ya uchunguzi iliyotolewa jana Jumamosi.

Ndege hiyo ya jeshi ilianguka wakati kulikuwa na utandu wa mawingu na upepo mkali Juni 10, 2024 na kusababisha majeraha kutokana na kasi ya juu yaliyoua wote waliokuwemo.

Ripoti hiyo ya tume maalum ilisomwa mubashara kwenye runinga.

Chilima, aliyekuwa na umri wa miaka 51, alikuwa maarufu sana nchini Malawi hasa kati ya watu wa umri wa chini, lakini uhusiano wake na Rais Lazarus Chakwera haukuwa mzuri.

Chama chake cha United Transformation Movement (UTM) kilidhihirisha wasiwasi kuhusu mazingira ya kifo cha Chilima na kuitisha uchunguzi.

Mwenyekiti wa tume hiyo ya uchunguzi Jabbar Alide ndiye alisoma ripoti hiyo ambapo alielezea kwamba marubani wawili wa ndege hiyo walipoteza uwezo wa kuona kufuatia utandu wa mawingu na upepo mkali.

Hali hiyo inasemekana kusababisha kila mmoja kufariki papo hapo na kwamba hakuna ushahidi wa mauaji au visababishi vingine vya vifo, kama vile kuumwa na wanyama.

Ripoti hiyo iliyosomwa kwa muda wa saa nne na nusu inafaa kuwasilishwa kwa Rais Chakwera.

Chilima alikuwa safarini pamoja na mke wa rais wa zamani Shanil Dzimbiri, kwenda kuhudhuria mazishi ya jamaa aliyekuwa waziri huko Mzuzu, umbali wa kilomita 370 kaskazini mwa jiji kuu Lilongwe, ajali ilipotokea.

Uchunguzi wa maiti za wahasiriwa ulibaini kwamba kila mmoja wao alikuwa na majeraha kwenye uso, kifua, miguu na mikono, ishara ya kurushwa kwa kasi dhidi ya vitu vugumu vilivyokuwa mbele yao kama viti.

Ndege hiyo ya jeshi la Malawi inaripotiwa kuacha shimo kubwa katika eneo ambalo ilianguka kutokana na kishindo na kisha kupasuka vipande vipande.

Chama cha Chilima cha UTM kilishirikiana na kile cha Chakwera cha Congress Party (MCP) kushinda uchaguzi wa urais mwaka 2020 lakini baadaye akatengwa.

Mwaka 2022 alikamatwa na kushtakiwa kwa kile kilochotajwa kuwa sakata ya hongo iliyohusisha mwanabiashara wa asili ya Malawi na Uingereza na hivyo kupokonywa mamlaka kama naibu rais.

Makosa hayo hata hivyo yalitupiliwa mbali mwezi mmoja tu kabla ya ajali hiyo ya ndege.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *