Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 10, Agnes Jebet Ng’etich, amesema analenga kunyakua medali katika mashindano ya Riadha Duniani mjini Tokyo, Japan.
Jebet alisema anapania kufungua msimu kwa kushiriki mbio za nyika za Sirikwa Classic tarehe 22 mwezi huu kabla ya kuelekea Jamaica mwezi wa nne na kisha ahudhurie majaribio ya kitaifa katika mbio za mita 5,000 na 10,000.
“Sina medali yoyote ya mashindano ya dunia, na mwaka huu hilo ndilo lengo langu; napania kushiriki mbio za mita 5,000 na 10,000 mjini Tokyo,” akasema Jebet.
Aidha Jebet, ambaye pia ndiye mwanariadha mwenye kasi zaidi katika mbio za nusu marathon, amewataka wanariadha kujiepusha na matumizi ya dawa kututumua misuli.
“Ninawaomba tu fellow athletes tukimbie clean; hakuja haja ya kutumia dawa kwa sababu tumeona wengi wamepigwa ban na kumaliza career zao.”
Jebet, aliye na umri wa miaka 22, aliweka rekodi mpya ya dunia ya kilomita 10 ya dakika 28 na sekunde 46 mjini Valencia, Uhispania, mwaka uliopita, na pia anajivunia kuwa mwanariadha mwenye kasi zaidi ya nusu marathon ya saa 1 dakika 3 na sekunde 4.
Mwanariadha huyo alikuwa akisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa makala ya nne ya mbio za nyika za Sirikwa Classic Cross Country Tour mjini Eldoret.