Afueni kwa wakazi wa Mtwapa kufuatia kuzinduliwa kwa hospitali

Dickson Wekesa
1 Min Read

Wakazi wa mji wa Mtwapa katika kaunti ndogo ya Kilifi Kusini wamepata afueni baada ya serikali ya kaunti ya Kilifi kuzindua hospitali ya kiwango cha nne eneo hilo.

Hii ni baada ya wakazi kuishi miaka mingi wakitegemea huduma za zahanati ya Mtwapa ambayo ilipandishwa cheo na kujengwa majengo ya kisasa na kuwekewa vifaa vya kisasa.

Wakazi hao watapata huduma mingi ikiwemo upasuaji, upimaji kwa kupigwa picha za eksirei na dawa na hawatalazimika kusafiri mwendo mrefu kupata huduma hizo.

Hospitali hiyo ina wodi mbili yenye vitanda 80 na inatazamiwa kuwapa wakazi huduma bora ambayo wamekuwa wakihitaji kwa muda mrefu.

Kulingana na Waziri wa Afya wa kaunti ya Kilifi Peter Mwarogo, serikali ya kaunti  inajizatiti kuiboresha sekta ya afya kupitia huduma bora katika hospitali hiyo.

Aidha Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro amesema serikali yake itajenga hospitali zaidi katika maeneo yote ili kuimarisha afya ya wakazi.

Mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo ya Mtwapa Godfrey Baraza alipongeza serikali ya kaunti kwa kuzingatia afya na kuiomba iwekeze vifaa zaidi.

Dickson Wekesa
+ posts
Share This Article