Afrika Mashariki yatakiwa kukumbatia maonyesho ya Karibu Kusini Iringa

Dismas Otuke
1 Min Read

Wakazi wa Afrika Mashariki wametakiwa kutumia fursa ya Maonyesho ya Utalii yatakayofanyika katika viwanja vya Kihesa Kilolo mkoani Iringa -Tanzania baina ya Septemba 23 hadi 27 mwaka huu.

Kwenye taarifa na wanahabari, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego amesema maonyesho hayo ya siku tano yatakuwa na shughuli mbalimbali kama vile kongamano la uwekezaji, utalii wa mitaani na tamasha ya utamaduni  katika mikoa yote 10.

Shughuli nyinginezo zitakuwa mbio za marathoni za hiari, kilomita 5 na kilomita 10, mbio za magari na pikipiki na maonyesho ya wanayama hai, utalii wa kamba na burudani.

“Lengo la maonyesho hayo ni pamoja na kuiishi kampeni ya the royal tour ilioanzishwa na rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Pamoja na kutangaza fursa za utalii na uwekezaji zilizopo kusini mwa Tanzania,” alisema Halima

Mikoa Kumi ya Kusini mwa Tanzania inatarajia Kushiriki maonyesho hayo yenye hadhi ya kimataifa.

Hafla hiyo itakamilika kwa kilele cha uadhimisho wa siku ya utalii ulimwenguni Septemba 27.

Tanzania ina vivutio vingi vya kitalii huku utalii ukiwa uti wa mgongo na kitega uchumi kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Share This Article