Afrika Mashariki iko tayari kuandaa kipute cha AFCON

Motsepe, alitoa hakikisho kuwa kamwe hadhamirii kupokonya Afrika mashiriki maandalizi hayo, hususan baada ya kuandaa fainali bora za CHAN mwaka jana.

Dismas Otuke
2 Min Read

Mataifa matatu wenyeji wa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2027, yamesema yako tayari kuandaa mashindano ya kufana.

Haya yalisemwa na viongozi wa serikali na mashirikisho ya soka matatu kutoka Kenya,Tanzania na Uganda, waliokutana Jumatatu Mei 11, katika kongamano la Africa Forward jijini Nairobi.

Waziri wa Michezo wa Uganda Moses Ogwang na mwenzake wa Kenya, Salim Mvyurya, walimhakikishia Rais wa CAF Patrice Motsepe, kuwa wako tayari kuandaa mashindano bora na ya kupigiwa mfano mwaka ujao.

“Serikali yetu ya Uganda imekuwa ikitoa kila msaada tunaohitaji kuandaa AFCON, na ningependa kukuhakikishia Rais kuwa Uganda haitakuangusha.”akasema Ogwang

Mvurya naye alisema”Mashindano yetu ya AFCON yatakuwa ya kihistoria na ya kukumbukwa kwani kila atakayehudhuria atajifunza kitu.”

Kauli za serikali pia ziliungwa mkono na mashirikisho ya soka kupitia kwa Marais wao,Hussein Mohamed wa Kenya,Moses Magogo wa FUFA na Wallace Karia wa TFF.

Upande wake kinara wa CAF, Motsepe, alitoa hakikisho kuwa kamwe hadhamirii kupokonya Afrika mashiriki maandalizi hayo, hususan baada ya kuandaa fainali bora za CHAN mwaka jana.

“Sina shaka kuwa Kenya,Uganda na Tanzania zitaandaa fainali bora baada ya kufanikisha fainali za mwaka jana za CHAN, wakati wengi walitilia shaka uwezo wa nchini hizi.”

Kenya,Uganda na Tanzania zitaandaa AFCON Juni 19 na Julai 17 mwaka ujao, zikiwa za mwisho kuandaliwa kila baada ya miaka miwili, kabla ya kuanza kwa mfumo wa miaka minne.

Share This Article