Afrika kutafuta suluhisho endelevu kwa janga la tabia nchi

Martin Mwanje
3 Min Read
Wakuu wa Nchi na Serikali wakati wa Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi katika jumba la KICC, Nairobi

Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka barani Afrika wamekubaliana kuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhisho endelevu kwa janga la tabia nchi.

Viongozi hao wamesema kuwa mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya bara hilo yanahusiana kwa karibu na hayawezi yakapuuzwa.

Walielezea dhamira yao ya kushirikiana na mataifa yaliyoendelea wakati pia wakiyakumbusha ahadi zao za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Wakiongozwa na mwenyeji wao Rais William Ruto wa Kenya, viongozi hao waliyasema hayo leo Jumanne wakati wa Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC jijini Nairobi.

Wao ni pamoja na Samia Suluhu (Tanzania), Paul Kagame (Rwanda), Évariste Ndayishimiye (Burundi), Filipe Nyusi (Msumbiji), Salva Kiir (Sudan Kusini), Sassou Nguesso (Congo) na Mostafa Madbouly (Misri).

Wengine ni Nana Akufo-Addo (Ghana), Mohamed Younis Menfi (Libya), Julius Maada (Sierra Leone), Sahle-Work Zewde (Ethiopia), Brahim Ghali (Sahrawi), Azali Assoumani (Comoros), Ismaïl Omar Guelleh (Djibouti), Isaias Afwerki (Eritrea) na Macky Sall (Senegal).

Rais Ruto alisema Afrika ilifanya uamuzi kimakusudi kuwa katika mstari wa mbele kutafuta suluhisho kwa tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema kulishinda tatizo hilo kutahitaji jitihada za pamoja kutoka kwa washikadau wote na mataifa.

“Hatuwezi tukakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia sera za kujikinga na za kibinafsi. Ongezeko la joto haliwezi likakabiliwa kwa kuweka viyoyozi kwenye vyumba vyetu vidogo na maeneo ya dunia.”

Rais Kagame alisema ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti zinazolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema kulaumiana siyo suluhisho.

“Mtazamo stahiki zaidi kwa Afrika ni kutekeleza jukumu kubwa katika utafutaji wa suluhisho za tabia nchi duniani,” alisema Rais Kagame.

Rais Suluhu alisema Afrika inapaswa kutumia wakati huu na uwezo wake kutoa suluhisho kwa ukuaji wa kijani na uondokanaji na kaboni.

“Hatuwezi kamwe tukamudu kuangazia maendeleo ya kiuchumi, mabadiliko ya tabia nchi na ufukara barani Afrika kwa kujitenga,” alisema Rais Suluhu.

Rais Akufo Addo alisema kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi barani Afrika.

“Ni wazi kwamba tunahitaji kuchukua hatua haraka na kwa njia thabiti kudhibiti athari hizi na kuhakikisha mustakabali endelevu kwa vizazi vijavyo,” alisema Rais Addo.

Kwa upande wake, Rais Afwerki alisema ni wakati wa Afrika kutafuta rasilimali zake badala ya kutegemea misaada.

Rais Zewde alitoa wito kwa Afrika nyakati zote kuchukua msimamo wa pamoja kuhusiana na masuala yanayowaathiri watu wake, akitaja mabadiliko ya tabia nchi.

Aliungwa mkono na Rais Kiir aliyesema Afrika ni lazima itumie rasilimali zake mbadala anuwai kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi lilianza jana Jumatatu na litafikia kikomo kesho Jumatano.

Wajumbe wapatao 30,000 wanashiriki kongamano hilo lililofunguliwa rasmi na Rais Ruto jana Jumatatu asubuhi.

Hilo ni kongamano la kwanza la aina hiyo kuwahi kufanyika.

Share This Article