Afisa mmoja wa polisi amefariki huku wenzake wawili wakijeruhiwa vibaya, baada ya idadi isiyojulikana ya wahalifu waliokuwa wamejihami kuwavamia katika eneo la Sessi, Moyale kaunti ya Marsabit.
Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi kaunti ya Marsabit Leonard Kimaiyo, alisema shambulizi hilo lilitekelezwa mwendo wa saa kumi na mbili Alhamisi jioni na wahalifu ambao walikuwa wakitumia piki piki.
Kimaiyo alisema maafisa wa asasi mbali mbali za usalama wameanzisha msako mkali dhidi ya wahalifu hao, ambao wanasemekana walikuwa wamejihamii kwa bunduki na guruneti.
Mwanamke mmoja anayeaminika kuwa mfanyakazi wa serikali ya kaunti ya Marsabit pia alijeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo.
Kimaiyo alisema waliojeruhiwa walipelekwa kwa matibabu katika hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Moyale ambapo afisa huyo wa polisi alifariki alipokuwa akipata matibabu.
Kamanda huyo pia alisema walinasa guruneti mbili mahala hapo.Maafisa hao wanatarajiwa kusafirishwa kwa ndege hadi hapa Nairobi kwa matibabu maalum.