Afisa mmoja wa usalama aliuawa, 305 walijeruhiwa wakati wa maandamano

Martin Mwanje
1 Min Read

Afisa moja wa usalama alifariki wakati wa maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Azimio. 

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo anasema jumla ya maafisa 305 walijeruhiwa vibaya wakati wakitekeleza jukumu lao kuu la kulinda maisha na mali.

“Idara ya polisi pia ilipoteza magari 158 na vituo vya polisi 9 ambavyo ama viliteketezwa au kharibiwa vibaya na wahalifu waliojisingizia kuwa wahalifu,” alisema Dkt. Omollo katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne.

“Maduka zaidi ya 850 na majengo mengine ya biashara pia yalivunjwa na kuporwa huku majengo 199 yakiharibiwa na taasisi mbalimbali za umma zenye thamani ya mabilioni ya pesa kuharibiwa.”

Kulingana na Dkt. Omollo, jumla ya visa 156 vya unyanyasaji na wizi wa mabavu pia viliripotiwa huku wenye magari ambao hawakuwa wanashiriki maandamano na watembea kwa miguu wakishambuliwa na kuporwa mali zao na waandamanaji walioziba barabara wakati wa maandamano.

Serikali inasema kwa sasa inachunguza ripoti za raia kubeba silaha na mchango wao kwa maafa yaliyoshuhudiwa wakati wa maandamano hayo.

Dkt. Omollo anasema kwa wakati huu, shabaha yao ni kurejesha amani na uthabiti nchini kupitia jitihada za pamoja, na anatoa wito kwa raia kudumisha utawala wa sheria na kuwasilisha lalama zao kupitia njia halali.

Website |  + posts
Share This Article