Afisa bandia wa NIS akamatwa kwa madai ya ufisadi

Tom Mathinji
1 Min Read
EACC wamkamata afisa bandia wa NIS kwa madai ya ufisadi.

Tume ya Maadili na vita dhidi ya Ufisadi (EACC), imemkamata afisa bandia wa Huduma ya Taifa ya  Ujasusi,  kwa kuhusika katika sakata ya utoaji zabuni ya shilingi milioni  15.

Kupitia kwa tarifa leo Alhamisi, tume hiyo ilisema kuwa uchunguzi wake umebainisha kuwa mshukiwa Joel Wanyama Simiyu, alijisingizia kuwa kuwa afisa wa NIS katika bodi ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF), na alitumia cheo hicho kuhadaa kampuni moja ya ujenzi kutekeleza ujenzi hewa katika shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika kaunti ndogo ya Hamisi, kaunti ya Vihiga.

Kulingana na EACC, ulaghai huo uligunduliwa wakati kampuni hiyo ilitaka malipo kutoka kwa afisi ya eneo bunge la Hamisi NG-CDF, huku ikibainika kuwa mradi huo ulikuwa tayari umeidhinishwa.

Baadaye mshukiwa huyo alijitokeza akiitisha hongo ya shilingi 20,000, akidai angefanikisha utoaji malipo hayo.

Maafisa wa EACC, walimkamata mshukiwa huyo akipokea mlungula huo na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central mjini Kisumu.

Baadaye aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 20,000, huku uchunguzi ukiendelea.

TAGGED:
Share This Article