Kenya imeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka ujao licha ya kutoka sare kwa kufungana bao 1-1 na Zimbabwe katika mechi ya Kundi J iliyochezwa Ijumaa jioni, kwenye Uwanja wa Peter Mokaba, Polokwane, Afrika Kusini.
Kenya ilikuwa inahitaji kushinda mechi hiyo ili ifuzu lakini bao lililofungwa na Tawanda Maswanhise liliiweka Zimbabwe kifua mbele katika kipindi cha kwanza.
Kenya ilisawazisha mechi hiyo kupitia kwa Jonah Ayunga katika dakika ya 52. Licha ya juhudi kubwa za kupata mshindi, Kenya haikuweza kuvunja ngome ya Zimbabwe na kulazimika kujipatia sare ambayo iliifuzisha Zimbabwe kwa fainali za kombe la bara Afrika mwaka 2025.
Kenya itamenyana na Namibia Jumanne ijayo katika mechi yake ya mwisho ya kundi J nchini Afrika Kusini ilihali Zimbabwe itacheza na vinara wa kundi J Cameroon.
Zimbabwe sasa inaungana na mataifa mengine kadhaa ambayo tayari yamefuzu kwa fainali za kombe la bara Afrika hatua ya fainali ya bara ikisalia na mechi moja.
Mataifa ambayo tayari yamefuzu kwa fainali hizo ni pamoja na: Wenyeji Morrocco,Uganda, Algeria,Tunisia,Afrika Kusini,Cameroon,Nigeria, Benin, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Angola miongoni mwa nyingine.