ADAK yakabiliwa na ukosefu wa fedha

Marion Bosire
2 Min Read
Naomi Waqo, mwenyekiti kamati ya michezo bungeni

Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli nchini, ADAK linakumbwa na tatizo la ukosefu wa fedha unaotokana na punguzo kubwa kwenye mgao wa bajeti.

Mkurugenzi Mtendaji wa ADAK Sarah Shibutse aliambia wanachama wa kamati ya michezo na utamaduni ya bunge kwamba wamejipata waliko kufuatia hatua ya Wizara ya Fedha ya kuwapunguzia mgao wa fedha.

“Shughuli za ADAK zimelemazwa na ufadhili wa kiwango cha chini kutoka kwa serikali,” alisema Shibutse kwenye kikao cha kamati hiyo chini ya uenyekiti wa mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Marsabit Naomi Waqo.

Aliongeza kwamba mmiliki wa jumba ambamo afisi zao ziko amewapa notisi wahame kwa kukosa kulipa kodi tangu mwezi Julai huku wakikatiziwa huduma za mtandao.

Shirika la ADAK vile vile linakabiliwa na wakati mgumu kulipa mishahara ya wafanyakazi wake na Shibutse anaomba mwingilio wa bunge.

Mgao wa ADAK ulipunguzwa hadi milioni 20 na anasema hatua hiyo imelemaza kabisa shirika hilo.

Alisema iwapo litashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, litajipata pabaya na Kenya kuwa katika hatari ya kutajwa kuwa isiyowajibika na Shirika la Kukabiliana na Dawa za Kusisimua Misuli Duniani, WADA.

Iwapo Kenya itatajwa kuwa isiyowajibika na WADA, Shibutse alisema madhara ni pamoja na kuzuiwa kwa wanariadha wa Kenya kushiriki mashindano ya kimataifa.

Kando na hilo, Kenya pia itakuwa katika hatari ya kunyimwa fursa ya kuandaa mashindano ya kimataifa kama vile CHAN na AFCON.

Shirika la ADAK lina jukumu la kuwafanyia vipimo wachezaji wa raga na voliboli wanaojiandaa kwa mashindano ya kimataifa hivi karibuni lakini ukosefu wa fedha huenda ukalemaza shughuli hiyo.

Kamati hiyo ya michezo ya bunge ilitambua matatizo ya ADAK na kutoa hakikisho kwamba suala hilo litashughulikiwa ipasavyo.

Itatafuta njia ya kuhakikisha kwamba hazina ya michezo nchini inatoa fedha kwa shirika hilo ili kulinusuru.

Charles Nguna, mwanachama wa kamati hiyo alikosoa Wizara ya Fedha kwa kupunguza mgao wa fedha kwa shirika la ADAK akisema kazi inayotekelezwa na shirika hilo ni muhimu.

Mwanachama mwingine Robert Basil alisema ADAK inastahili kuwa huru.

Share This Article