Wadau katika sekta ya utalii nchini wamelalamikia nyongeza mpya ya ada za kuzuru mbuga za wanyama nchini iliyotangazwa na serikali kuanzia Januari 1 mwaka ujao wakisema kuwa huenda ikapunguza idadi ya watalii wanaoingia nchini.
Msimamizi katika kampuni ya safari za kitalii ya Crowned Eagle Safaris, David Iteyo amesema serikali kupitia Wizara ya Utalii ilipaswa kuongeza ada hizo kwa awamu badala ya kuongeza kwa zaidi ya asilimia 150 kwa mkupuo.
Iteyo pia ameelezea haja ya serikali kushauriana na wadau katika sekta hiyo kabla ya utekelezaji wa ada hizo mpya akisema huenda Kenya ikapoteza watalii wengi kwa taifa jirani la Tanzania.
“Ada hizi mpya zilizopendekezwa ambazo ni zaidi ya asilimia 150 nahofia huenda zikawatishia watalii wengi wanaozuru nchini na ambao huenda wakaelekea kwa majirani zetu Tanzania. Ingekuwa bora iwapo hii nyongeza ya ada mpya ingetekelezwa kwa awamu badala ya mara moja,” alishauri Iteyo.
Ada hizo mpya zitaathiri watalii wote wa kigeni na raia wa humu nchini wanaopania kuzuru mbuga na maeneo ya kitalii kuanzia Januari mosi mwaka 2024.
kulingana na malipo mapya yaliyopendekezwa na shirika la uhifadhi wanyamapori, KWS, kuanzia Januari mosi mwaka ujao, watalii wa humu nchini watalipa shilingi 2,000 kuzuru mbuga za wanyama msimu wenye idadi kubwa ya watalii kati ya Julai na Machi kutoka ada za sasa za shilingi 430.
Mtalii kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki watalipia dola 50 huku watalii wa mataifa mengine ya kigeni wakilipa dola 100 za Marekani.