Abba Marcus Ssali kifungua mimba wa mwanamuziki wa Uganda Joseph mayanja maarufu kama Jose Chameleone amewatupia maneno makali wakosaji wake.
Usiku wa Jumapili Disemba 29, 2024, Marcus aliangazia watu kadhaa maarufu nchini Uganda wakiwemo waandalizi wa matamasha Bajjo na Abitex, na watangazaji Miles Rwamiti na Roger Otis.
Marcus alimtaja Abitex kuwa “mjinga” baada yake kudai kwamba yeye ni mtoto mdogo sana ambaye hafai kukosoa wazazi wake na babu na nyanyake.
Wakati wa mahojiano Abitex alidai kwamba mamake Marcus kwa jina Daniella Atim, sio mwanamke wa kwanza kutalikiwa au kupitia dhuluma.
Kwa hilo Marcus alimjibu akisema yeye ni mjinga ambaye anajaribu kuhalalisha dhuluma za kijinsia katika ndoa.
Marcus amengaziwa na wengi wakiwemo watangazaji hao, baada yake kudai kwamba babake anasumbuliwa ba matumizi mabaya ya pombe ambayo yamemsababishia ugonjwa wa kongosho.
Katika video aliyochapisha kwenye Tiktok, Marcus alilaumu babu na nyanyake kwa kile alichokitaja kuwa kutowajibika na kudhibiti unywaji pombe wa babake.
Wakati huo Jose Chameleone alikuwa amelazwa hospitalini nchini Uganda kabla ya kuhamishiwa hospitali moja nchini Marekani.
Baada ya ufichuzi wa maradhi ya babake, Marcus alijitokeza tena kudai kwamba Jose Chameleone alikuwa amekatiza mawasiliano naye.
Mjombake aitwaye Douglas Mayanja ambaye aliandamana na Jose Chameleone kwenda Marekani naye alilalamikia ufichuzi wa Marcus akiutaja kuwa udhalilishaji.
Kulingana na Douglas ambaye anafahamika zaidi kama Weasel Manizo, Marcus hafai kuchafulia babake jina ikitizamiwa kwamba amekuwa akimlipia karo ya shule ambayo ni ghali mno nchini Marekani.
Marcus alijibu hilo akisema babake ahafai kusifiwa kwa kumlipia karo kwani ni wajibu wake kama mzazi.