Waigizaji wa muda mrefu nchini Tanzania Irene Uwoya, Aunty Ezekiel, Fridah Kajala na Jacqueline Wolper ambao wanaendesha kipindi kuhusu maisha yao cha A List, wameitwa na Bodi ya Filamu ya Tanzania, TFB.
Katika chapisho kwenye akaunti rasmi ya Instagram, TFB iliweka ilani ya kuwataka wanne hao kufika kwenye afisi za bodi leo Septemba 7, 2026 saa nane mchana.
Ingawa ilani hiyo haina maelezo ya ndani, inaaminika wito huo umetokana na maudhui kwenye kipindi chao cha A List kinachopeperushwa na Maisha Magic Bongo.
Kulingana na maelezo ya Maisha Magic Bongo, kipindi hicho kinahusu kufunguka kwa wanne hao kusema ukweli wao, kuzungumzia urafiki wao na changamoto za kibinafsi.
Nyota hao wa uigizaji wamekuwa wakifichua na kujadili mambo ya ndani kuwahusu ikiwemo aliyebikiri kila mmoja wao huku Uwoya akimtaja Ali Kiba.
Wamejadili pia utata uliozunguka uhusiano wa kimapenzi wa Kajala na Harmonize ambapo Harmonize alilaumiwa kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kajala na binti yake Paula.
Maudhui hayo yamezua mjadala mkali kati ya wanaotumia mitandao nchini Tanzania ambapo wengi wanahisi kwamba hayakidhi maadili na huenda ndiyo sababu yao kuitwa na bodi ya filamu.
Wito huo wa TFB unafuatia wito wa hivi karibuni wa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Patrobas Katambi, kwa wasanii na watayarishaji wa maudhui nchini Tanzania kuwajibika zaidi wanapotumia mitandao ya kijamii na kuzingatia sheria za nchi.