Wakazi wa eneo la Ntharene kaunti ndogo ya Imenti Kusini kaunti ya Meru wamefanya maandamano ya amani leo, kulalamikia kubanduliwa mamlakani kwa Gavana wa kaunti hiyo Kawira Mwangaza na wanachama wa bunge la kaunti ya Meru.
Wakazi hao wanasema hatua ya kumwondoa gavana Mwangaza mamlakani ni suala la siasa ambalo wanaamini lilichochewa na seneta wa kaunti hiyo Kathuri Murungi na waziri wa kilimo Mithika Linturi.
Wakazi hao sasa wanataka Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua kuingilia kati na kumwokoa gavana huyo wakiongeza kwamba wakazi wote wa kaunti hiyo wanaunga mkono uongozi wake.
Walisema iwapo kubanduliwa kwa gavana Kawira Mwangaza kutaidhinishwa na bunge la Seneti, basi Rais anafaa kufikiria kuvunja serikali nzima ya kaunti ya Meru inayojumuisha bunge la kaunti.
Wakazi hao walisisitiza kwamba wana imani kabisa na kiongozi huyo wao Kawira Mwangaza ndiposa wakajitokeza kwa wingi kumpigia kura kumchagua kama gavana wa kaunti ya Meru kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
Gavana Kawira Mwangaza alibanduliwa mamlakani kwa mara ya pili na wabunge wa bunge la kaunti ya Meru Oktoba 25, 2023.
Wawakilishi wadi 59 kati ya wote 69 walipiga kura ya kuunga mkono kuondolewa kwake mamlakani na 10 waliosalia hawakufika bungeni kupiga kura.