Filamu Utata kuzinduliwa Disemba huko Mombasa

Filamu hiyo imechochewa na historia ya Nusaybah bint Ka'ab, mwanamke Mwislamu aliyesifika kwa ushujaa.

Marion Bosire
1 Min Read

Mtayarishaji filamu maarufu wa Kenya, Daudi Anguka, anajiandaa kuzindua filamu yake mpya kwa jina “Utata”, inayohusu siasa na mapambano, Desemba 19, 2026, huko Fort Jesus, Mombasa.

Filamu hiyo iliyotayarishwa na AR Films na kuongozwa na ushirikiano wa Anguka na Eric Mdagaya, inatarajiwa kuwa mradi wa Anguka mkubwa baada ya mafanikio ya filamu yake ya “Mvera”.

Ikiwa imeandaliwa katika mazingira ya Pwani ya Kenya, Utata inasimulia kisa cha Tanim Samira, anayeigizwa na Deeja Omondi, ambaye ni mwanamke Mwislamu anayehusika na ulinzi wa karibu wa Gavana wa Mombasa.

Baada ya kuzuia jaribio la kumuua gavana huyo, anagundua njama inayomhusisha kiongozi huyo na kuingizwa kwa vijana wa Pwani katika itikadi na misimamo mikali.

Uchunguzi wake unakuwa wa kibinafsi anapogundua kuwa kakake aliyepotea kwa muda mrefu anahusishwa na matukio hayo, jambo linalomweka katika njia panda kati ya kulipiza kisasi na kutafuta haki.

Filamu hiyo imechochewa na historia ya Nusaybah bint Ka’ab, mwanamke Mwislamu aliyesifika kwa ushujaa.

Waigizaji wengine kwenye filamu hiyo ni Patrick Owino, Isarito Mwakalindile, Mariah Ahmed, Nima Kubo na Said Muhsin. Alice Wahome ni mtayarishaji mwenza mkuu.

Mapokezi ya wageni kwenye zulia jekundu yataanza saa 11 jioni, kabla ya maonyesho rasmi. Tiketi zinapatikana kupitia Gatepass Tickets.

Share This Article