Jamaa mmoja anayejulikana kwa kupokea na kuhifadhi simu za mkononi zilizoibwa amekamatwa katika eneo la Mowlem, Nairobi.
Haya yanafuatia operesheni iliyoongozwa na taarifa za kijasusi iliyofanywa na maafisa wa upelelezi kutoka Dandora.
Mshukiwa huyo, Patrick Muthui, alikamatwa katika eneo la Tononoka baada ya wapelelezi kupata taarifa zilizowaongoza moja kwa moja hadi kwenye maficho yake.
Msako uliofanywa katika eneo hilo ulifichua simu nyingi za mkononi zilizokuwa zimetenganishwa vipande, pamoja na vifaa vya kielektroniki vilivyotumika kufungua simu na kubadili nambari zake za utambulisho za IMEI.
Vitu vyote vilivyopatikana vimehifadhiwa kama vielelezo vya ushahidi, huku mshukiwa akiendelea kuzuiliwa na polisi kwa ajili ya taratibu za kisheria kabla ya kufikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, maafisa wa upelelezi wanaendelea kufuatilia vidokezo zaidi ili kubaini wamiliki halali wa simu zilizopatikana.