Ruto akubaliana na wito wa Zimbabwe

Zimbabwe inataka kuondolewa vikwazo na kurejeshwa kwenye jumuiya ya madola.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesisitiza kuwa Kenya inaunga mkono juhudi za Zimbabwe kurejeshwa katika Jumuiya ya Madola.

Kiongozi wa nchi anataka pia vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya taifa hilo la kusini mwa Afrika viondolewe mara moja na bila masharti.

Akizungumza katika mkutano na Rais wa Zimbabwe na ujumbe wake katika ikulu ya Nairobi, Ruto alitaja vikwazo hivyo vya upande mmoja kuwa visivyo vya haki na visivyo vya lazima kwani vinaathiri zaidi wananchi wa kawaida, hasa makundi yaliyo katika mazingira magumu.

Alisisitiza kuwa hatua hizo zinadhoofisha mamlaka na uhuru wa Zimbabwe, akirudia msimamo wa Kenya kwamba vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa bila masharti yoyote.

Kauli za Ruto zilitolewa wakati wa majadiliano mapana kuhusu kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kutetea maslahi ya Afrika katika masuala ya kimataifa, wakati wa kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kenya na Zimbabwe.

Viongozi hao wawili pia walithibitisha dhamira yao ya kuimarisha umoja wa Afrika na ushirikiano wa kikanda, huku Kenya ikiahidi kuunga mkono uongozi wa Zimbabwe katika Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika, COMESA.

Ruto aliipongeza Zimbabwe kwa kuchaguliwa kuwa mjumbe asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2027 hadi 2028, akisema nafasi hiyo itatoa fursa ya kuendeleza suluhisho la migogoro yanayoongozwa na Waafrika.

Kenya na Zimbabwe pia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zao za ulinzi na usalama katika kukabiliana na ugaidi, uhalifu wa kupangwa na vitisho vya kiusalama vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Share This Article