Aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Migori Okoth Obado,amehukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.
Mahakama Kuu ya Milimani, imemhukumu Obado pamoja na washtakiwa wenza wawili kuhusiana na mauaji hayo yaliyotekelezwa mwaka 2018.
Akitoa hukumu hiyo siku ya Ijumaa, Lady Justice Cecilia Githua alibainisha kuwa Obado na washtakiwa wenza Michael Juma Oyamo aliyekuwa msaidizi wa Obado, na Caspal Ajwang Obiero aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori, na wengine ambao hawakuwa mahakamani, walishirikiana kutekeleza uhalifu huo.
Oyamo amehukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa kuhusika moja kwa moja katika kuratibu na kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, huku Obiero akihukumia miaka 18 gerezani.
“Baada ya kuchunguza kwa makini ushahidi uliowasilishwa, ni bayana kwamba washtakiwa walishirikiana na wengine ambao hawako mahakamani kutekeleza uhalifu huo,” alisema Jaji huyo.
Mahakama ilisema Obado alitoa wazo hilo la mauaji na ufadhili wa rasilimali kutekeleza mauaji hayo, huku Oyamo akishirikisha utekelezwaji waki, naye Obiero akitoa usaidizi wa usafiri na kuficha uhalifu huo.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 42 kwenye kesi hiyo.
Watatu hao walikuwa wamepatikana na hatia ya mauaji hayo mnamo Julai 23, 2026, kufuatia kesi iliyochukua muda mrefu tangu Sharon Otieno—ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi saba—alipotekwa nyara na kuuawa mnamo Septemba 2018.