Rais Ruto aidhinisha miswada kadhaa kuwa sheria

Inalenga kuimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma, kuboresha mafao ya kustaafu, kulinda kina mama wanaonyonyesha na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa waathiriwa wa dhuluma za kingono.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ametia saini na kuidhinisha kuwa sheria, miswada kadhaa inayolenga kuimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma. 

Inalenga pia kuboresha mafao ya kustaafu kwa wafanyakazi, kulinda kina mama wanaonyonyesha na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa waathiriwa wa dhuluma za kingono.

Miswada hiyo ni Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki wa mwaka 2026, unaotaka Bunge la Kitaifa kuidhinisha matumizi ya fedha za umma kwa benki hiyo kabla ya fedha hizo kutolewa, pamoja na idhini ya Mdhibiti wa Bajeti.

Mswada wa Marekebisho ya Mpango wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma wa mwaka 2025 unapendekeza kuruhusu wafanyakazi walioajiriwa kwa mikataba ya muda maalumu kujiunga na hazina ya pensheni, kuweka akiba ya ziada kwa hiari na kunufaika na huduma nyingine, zikiwemo za matibabu baada ya kustaafu na mikopo ya nyumba.

Mswada wa Kina Mama Wanaonyonyesha wa mwaka 2024 unawataka waajiri kutoa vyumba maalumu vya faragha kwa ajili ya kunyonyesha au kukamua maziwa, pamoja na mapumziko yanayofaa. Pia unapiga marufuku ubaguzi unaohusiana na ujauzito na unyonyeshaji.

Mswada wa Taasisi ya Wataalamu wa Mazingira nchini Kenya wa mwaka 2024 unaweka mfumo wa kusajili na kutoa leseni kwa wataalamu wa mazingira.

Aidha, marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Kingono yanalenga kuongeza uhamasishaji wa umma na kulinda haki ya waathiriwa kupata elimu.

Marekebisho mengine yanapiga marufuku usuluhishaji wa kesi za makosa ya kingono nje ya mahakama na yanataka kesi hizo kukamilishwa ndani ya miezi sita tangu mshtakiwa afikishwe mahakamani kujibu mashtaka.

Miswada hiyo ilipitishwa na Bunge la Kitaifa mwezi Oktoba na Novemba 2026 kabla ya kuwasilishwa kwa Rais kwa ajili ya kuidhinishwa.

Share This Article