Mchungaji na mwanamuziki maarufu wa nyimbo za Injili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Emmanuel Ushindi Kamundala, anayefahamika zaidi kupitia wimbo wake maarufu wa ‘Dunda Mu Yesu’ amefariki.
Ushindi aliaga dunia mjini Bunia, katika jimbo la Ituri nchini DRC, usiku wa kuamkia jana Jumatano, Novemba 25, 2026.
Kifo chake kilitokea siku chache baada ya kukamilisha kampeni ya wiki moja ya uinjilisti katika kanisa moja la Kipentekoste mjini Bunia, Jumatatu, Novemba 23.
Ingawa taarifa zinathibitisha kuwa alifariki mjini humo, kuna taarifa zinazokinzana kuhusu mahali mwili wake ulipatikana.
Taarifa kutoka kwa familia yake zilisema alipatikana nyumbani kwake, huku ripoti nyingine zikidai alipatikana katika chumba cha hoteli katika eneo la Mbunya alipokuwa akitekeleza shughuli za uinjilisti.
Mamlaka bado hazijathibitisha rasmi chanzo cha kifo chake huku uchunguzi ukiendelea.
Ushindi, ambaye pia alifahamika kwa jina la Chabusiku, alitokea eneo la South Kivu na pia aliwahi kuishi Nairobi, Kenya.
Alijijengea umaarufu mkubwa Afrika Mashariki na Kati kupitia nyimbo za Injili za Kiswahili zikiwemo ‘Heshimu Wazazi’ na ‘Uheshimiwe Baba’.
Wasanii wenzake wa nyimbo za Injili na mashabiki wa Kenya na DRC wameendelea kutoa salamu za rambirambi, wakikumbuka huduma yake ya kiroho na mchango wake katika muziki wa Injili.