Rebekah Dawn apata uraia wa Kenya

Alitangaza hatua hiyo kupitia mitandao ya kijamii Jumatano, Novemba 25, 2026, baada ya miongo kadhaa ya kuishi, kuhudumu kidini na kulea familia yake nchini Kenya.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili na kiongozi wa ibada mzaliwa wa Marekani, Rebekah Dawn, amepata rasmi uraia wa Kenya, hatua inayothibitisha uhusiano wake wa muda mrefu na nchi hii ambayo amekuwa akiishi tangu akiwa mchanga.

Dawn alitangaza hatua hiyo kupitia mitandao ya kijamii Jumatano, Novemba 25, 2026, baada ya miongo kadhaa ya kuishi, kuhudumu kidini na kulea familia yake nchini Kenya.

Alizaliwa huko Centerville, Mississippi, nchini Marekani, na kuhamia Nairobi akiwa na umri wa miezi sita pamoja na wazazi wake waliokuwa wamishonari.

Isipokuwa kwa vipindi vifupi alivyokaa nje ya nchi, ikiwemo miezi 10 nchini Marekani alipokuwa katika mwaka wake wa mwisho wa shule ya upili na mwaka mmoja wa masomo ya huduma ya muziki nchini Australia, Dawn amekulia Kenya karibu maisha yake yote.

Kabla ya kupata uraia rasmi, mwimbaji huyo alikuwa akijitambulisha kama Mkenya moyoni na kwa ndoa, baada ya kufunga ndoa na mwanamuziki wa Kenya Allan Gituthu, maarufu kama Allan Sucre, Desemba 2015.

Dawn anahudumu kama Mkurugenzi wa Sanaa na kiongozi wa ibada katika kanisa la Nairobi Lighthouse.

Amekuwa jina maarufu katika tasnia ya muziki wa injili Afrika Mashariki, akipendwa kwa nyimbo zake za ibada anazoimba kwa ufasaha wa Kiswahili, zikiwemo “Kutembea Nawe” na “Nitakumbuka”.

Share This Article