Bunge lamulika punguzo la bajeti ya idara ya ardhi

Mgao wa idara hiyo unapendekezwa kupunguzwa kutoka shilingi bilioni 17.14 za mwaka wa kifedha wa 2026/27 hadi bilioni 14.81.

Marion Bosire
1 Min Read
Joash Nyamoko, Mwenyekiti, Kamati ya Bunge la Kitaifa Kuhusu Ardhi

Kamati ya Bunge la Kitaifa Kuhusu Ardhi, imeibua wasiwasi kuhusu pendekezo la kupunguza bajeti ya Idara ya Ardhi na Mipango ya Kimaeneo kwa shilingi bilioni 2.33.

Taasisi hiyo inaonya kwamba hatua hiyo huenda ikadhoofisha utoaji huduma na mageuzi yanayoendelea.

Wasiwasi huo uliibuka wakati Katibu Mkuu wa Idara hiyo Nixon Korir, akiwasilisha taarifa ya Bajeti ya mwaka 2027 mbele ya kamati inayoongozwa na Mbunge Joash Nyamoko.

Korir alisema mgao wa idara hiyo unapendekezwa kupunguzwa kutoka shilingi bilioni 17.14 za mwaka wa kifedha wa 2026/27 hadi bilioni 14.81.

Fedha za maendeleo ndizo zimeathirika zaidi, zikipunguzwa kutoka shilingi bilioni 11.41 hadi shilingi bilioni 8.86, hali inayoweza kuathiri uwekaji wa kumbukumbu za ardhi kidijitali, mipango ya makazi na ujenzi wa ofisi za ardhi.

Mgao huo unajumuisha bilioni 4.723 za makazi ya watu wasio na ardhi, utoaji wa hati miliki na kuwahamisha walioathiriwa na miradi ya maendeleo, kikiwemo kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote kinachopendekezwa Lamu.

Wabunge Omar Mwinyi na Fatuma Jehow walitilia shaka usambazaji wa miradi kikanda, wakitaka utekelezaji wa mpango wa Usawa Ni Sawa uzingatie haki na usawa.

Korir alitaja uhaba wa wafanyakazi, madeni ya hukumu za mahakama na kucheleweshwa kwa upimaji wa ardhi kama changamoto zinazohitaji ufadhili zaidi.

Share This Article