Wakulima wa miwa waanza kupokea bonasi ya shilingi bilioni 1.2

Ili kufufua sekta ya sukari nchini Kenya, Ruto alisema serikali ilifutilia mbali deni la shilingi bilioni 117, lililokuwa likidaiwa na kampuni za kusaga miwa.

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto azindua malipo ya bonasi kwa wakulima wa miwa, katika kiwanda cha Nzoia kaunti ya Bungoma.

Rais William Ruto leo Jumamatu amezindua zoezi la kuwalipa wakulima wa miwa  bonasi, ya kitita cha shilingi bilioni 1.2.

Akizungumza katika kiwanda cha kusaga miwa cha Nzoia kaunti ya Bungoma, kiongozi wa taifa alisema wakulima ambao huuza miwa yao katika kiwanda hicho, walipokea shilingi milioni 195, akidokeza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha wakulima wanafaidika pakubwa kutokana na kilimo chao.

“Juma lijalo, wakulima wa kiwanda cha sukari cha Mumias , kaunti ya Kakamega, pia watapata bonasi. Sawia na wale wa  Chemilil (Kisumu), Muhoroni (Kisumu) na Sony kaunti ya  Migori,” alisema Rais Ruto.

Kulingana na Rais Ruto, serikali yake imetimiza ahadi za kufanyia mabadiliko ukulima wa miwa kwa njia tofauti, ikiwa ni pamoja na kukodisha viwanda vya umma kwa sekta ya kibinafsi, na wakulima wanalipwa kila wiki baada ya kuwasilisha miwa yao.

“Wafanyakazi pia wanalipwa kila mwezi,” aliongeza Rais Ruto.

Ili kufufua sekta ya sukari nchini Kenya, Ruto alisema serikali ilifutilia mbali deni la shilingi bilioni 117, lililokuwa likidaiwa na kampuni za kusaga miwa, huku ikihakikisha wakulima wanapata mbolea ya bei nafuu.

“Kutokana na hayo, uzalishaji wa sukari umeongezeka na mwaka huu unatarajiwa kufika metrik tani 900,000, na tunalenga kufika metrik tani milioni 1.2, ili Kenya iweze kuwa na utoshelevu wa sukari,” aliongeza Rais Ruto.

TAGGED:
Share This Article