Kiongozi wa chama cha PNU, Peter Munya, ametaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, idhihirishe uhuru wake na kuzingatia uwazi huku nchi ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027.
Akizungumza katika eneo bunge la Othaya, Munya alisisitiza umuhimu wa mchakato wazi na wa kuaminika katika kuajiri Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo.
Alisema imani ya wananchi kwa IEBC inategemea uwezo wake wa kufanya kazi bila kuingiliwa na kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.
Kwa upande wa siasa, Munya amesema viongozi wa vyama vinavyoshirikiana katika muungano wa upinzani wanaendelea na mazungumzo ya kutafuta mgombea mmoja wa urais atakayemkabili Rais William Ruto katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Hata hivyo, Gavana huyo wa zamani wa Meru amekosoa kaulimbiu ya Rais Ruto ya ‘Usawa ni Sawa’, akiishutumu serikali yake kwa kile anachodai kuwa ni ugawaji wa nafasi za ajira serikalini unaopendelea baadhi ya makabila.
Munya anasema tofauti hizo zinazodaiwa zinaweza kudhoofisha umoja wa kitaifa na kuwanyima baadhi ya Wakenya fursa sawa za kupata ajira katika utumishi wa umma.