Mutua akutana na mashirika ya ajira ughaibuni

Walijadili mpango wa majaribio wa miezi mitatu wa kurahisisha upatikanaji wa ajira kwa Wakenya nchini Saudi Arabia.

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii, Alfred Mutua, amefanya mazungumzo na mashirika ya ajira ughaibuni nchini Kenya.

Walijadili kuhusu mpango wa majaribio wa miezi mitatu unaolenga kurahisisha upatikanaji wa ajira kwa Wakenya nchini Saudi Arabia.

Mutua alisema mkutano huo uliofanyika jijini Nairobi ulikutanisha wawakilishi wa mashirika ya uajiri yanayotaka kushiriki mpango huo.

Mazungumzo hayo yanafuatia mikutano ya hivi karibuni kati ya Kenya na Saudi Arabia jijini Riyadh, ambapo serikali za nchi hizo mbili zilitia saini barua ya makubaliano ya nia ya kuimarisha ushirikiano katika masuala ya ajira, kupanua fursa za kazi na kuhakikisha uhamiaji wa wafanyakazi unafanyika kwa usalama na uwazi.

Mutua alisema mashirika hayo yalielekezwa kuhusu malengo ya mpango huo, mfumo wa utekelezaji na masharti ya kushiriki.

Walijadili pia usajili wa mashirika, utayari wa vituo vya uchunguzi wa afya, nyaraka na uchakataji wa visa.

Aliyahimiza mashirika yanayotaka kushiriki, kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira, NEA, na kutimiza masharti yote ya kisheria.

Waziri huyo pia aliwaonya Wakenya wanaotafuta ajira nchini Saudi Arabia dhidi ya kutumia mashirika yasiyoidhinishwa au kukubali matangazo ya kazi ambayo hayajathibitishwa, akiwataka kuwa waangalifu dhidi ya matapeli.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEA, Edith Okoki, Mkurugenzi wa Uhamiaji wa Wafanyakazi Joseph Njue pamoja na maafisa wengine wa serikali.

Share This Article