Viongozi wa upinzani wajiondoa mkutano na IEBC

Wanadai kwamba tume hiyo imekosa kushughulikia masuala waliyoibua kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 10, 2027.

Marion Bosire
2 Min Read

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua wameikosoa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, baada yao wenzao kujiondoa kwenye mkutano na maafisa wa tume hiyo.

Wanadai kwamba tume hiyo imekosa kushughulikia masuala waliyoibua kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 10, 2027.

Katika taarifa tofauti walizochapisha kwenye mitandao ya kijamii leo Alhamisi, Novemba 19, viongozi hao walitilia shaka uhuru, maandalizi na utayari wa tume hiyo kushirikiana na wadau katika masuala ya mageuzi ya uchaguzi.

Kalonzo alisema upinzani ulihudhuria mkutano huo kwa nia njema lakini haukuridhishwa na kile alichokitaja kuwa ukosefu wa kutopendelea upande wowote na maandalizi ya kutosha kwa upande wa IEBC.

Alionya kuwa upinzani hautashiriki katika mijadala inayoweza kuhalalisha uchaguzi alioutaja kuwa uliopangwa kuwa na udanganyifu, akisisitiza kuwa kila kura lazima ihakikiwe hadharani na kutangazwa jinsi ilivyopigwa katika vituo vya kupigia kura.

Kwa upande wake, Gachagua aliishutumu IEBC kwa kupuuza maombi ya mara kwa mara ya viongozi hao ya kutaka mazungumzo na ufafanuzi kuhusu masuala yaliyoibuliwa na Wakenya.

Alisisitiza kuwa hakuna maamuzi ya uchaguzi yanayopaswa kufanywa bila ushiriki wa wananchi, akitaka tume hiyo kusikiliza maoni yao kabla ya upinzani kurejea kwenye mazungumzo.

Viongozi wengine waliohusika katika msimamo huo ni Fred Matiang’i, Martha Karua, Justin Muturi, Eugene Wamalwa, Edwin Sifuna na David Maraga, ambao wanataka mchakato wa uchaguzi ulio huru na wa kuaminika.

Share This Article