Rais William Ruto ametoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa duniani kote kuhakikisha kila mtu anapata chakula bora chenye lishe na kinachotosheleza.
Amehusisha njaa ambayo imekuwa ikishuhudiwa duniani kote na hatua zisizotosheleza zinazochukuliwa na mamlaka husika.
“Dunia tayari inazalisha chakula cha kutosha cha kumlisha kila mtu. Kwa miongo kadhaa, njaa imechochewa kwa kiwango kidogo na uhaba mkubwa wa chakula bali hatua tunazochukua: kile tunachofadhili, tunachojenga, nani tunayemlinda na fursa tunazobuni,” alisema Rais Ruto.
“Hivyo jukumu letu siyo tu kuzalisha chakula zaidi, bali kuhakikisha kuwa kila mtu anaweza akapata chakula cha kutosha, salama, cha bei nafuu na chenye lishe.”
Alililamikia idadi kubwa ya watu wasioweza kupata chakula bora ikiwa takriban asilimia 2.7 huku idadi hiyo ikiwa karibu watu wawili kati ya kila watu watatu barani Afrika.”
“Ikiwa njaa huchochewa na hatua za umma, basi kuimaliza kunahitaji sheria, bajeti na uangalizi. Haya ni miongoni mwa majukumu muhimu ya mabunge.”
Rais Ruto alyasema hayo leo Jumatatu wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa wabunge kuhusu njaa na utapiamlo.
Mkutano huo wa siku mbili unafanyika katika majengo ya Bunge jijini Nairobi.
Nao unakutanisha wabunge zaidi ya 250 na wadau wa maendeleo kutoka mabunge mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili mikakati ya kukabiliana na njaa na utapiamlo.
Huu ni mwaka wa kwanza kwa mkutano huo wa kimataifa kufanyika barani Afrika.
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amekuwa akisimamia maandalizi ya mwisho ya mkutano huo kwa kushirikiana na wabunge, wasimamizi wa bunge na wafanyakazi wengine.
Mkutano huo unaandaliwa kwa pamoja na Bunge la Kenya, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na Shirika la Uhispania la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa, AECID.
Washiriki wanatarajiwa kujadili hatua za kisheria, kibajeti na kiusimamizi zitakazosaidia kuimarisha uwepo wa chakula cha kutosha, kuboresha lishe na kuhakikisha wananchi wanapata haki ya chakula kupitia maendeleo jumuishi na mifumo endelevu ya kilimo.
Mazungumzo yataangazia pia changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na kuyumba kwa uchumi.
Mkutano wa Nairobi unajengwa juu ya mikutano iliyotangulia ya Madrid, Uhispania, mwaka 2018 na Valparaíso, Chile, mwaka 2023.