Msanii mkongwe wa Bongo Fleva Q Chief, amesema amesuluhisha tofauti zake na msanii mwenzake T.I.D, baada ya kupokea simu yake ya kuomba msamaha.
Q Chief ambaye jina lake halisi ni Abubakar Shaban Katwila anasema kwamba alikubali msamaha wa TID au ukipenda Khalid Mohamed, bila kujali iwapo ombi hilo lilitoka moyoni au la.
Alisema licha ya kuwa na mitazamo tofauti, binadamu wana nafasi ya kuchagua kati ya ukatili na moyo wa wema, akieleza kuwa yeye ameamua kusamehe.
Wawili hao wamekuwa na historia ndefu ya urafiki na migogoro iliyodumu kwa miaka kadhaa, huku wakiripotiwa kufanya juhudi mbalimbali za kurejesha uhusiano wao.
Katika hatua nyingine, Q Chief amesema Tamasha ya Miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva imekuwa na mchango chanya katika kufufua maisha yake ya muziki.
Pia amewashukuru waandaaji wa tamasha hiyo, Madee Ali na Babu Tale, kwa kuwapa wasanii wakongwe fursa ya kurejea kwenye majukwaa na kuonyesha vipaji vyao baada ya kipindi ambacho baadhi yao walionekana kupoteza nafasi katika tasnia ya muziki.