Serikali imo mbioni kuajiri walimu 20,000 zaidi mwezi ujao wa Desemba ili kukabiliana na uhaba wa walimu ambao umekuwa mwiba kwa sekta ya elimu nchini kwa miaka mingi iliyopita.
Rais William Ruto amesema serikali ya Kenya Kwanza tayari imeajiri walimu 100,000 tangu ilipoingia madarakani wakati madarasa 23,000 yakijengwa.
Ruto amesema chini ya utawala wake, walimu pia wamepandishwa ngazi wakati maslahi yao yakitiliwa maanani katika jitihada za kuboresha viwango vya elimu vinavyotolewa nchini.
“Tunajenga mfumo wa elimu unaoandaa watoto wetu kwa dunia watakayorithi, tukiwapa maarifa, ujuzi na umilisi wa kufikiria kiubunifu, kutatua matatizo na kugeuza mawazo kuwa suluhu za kivitendo,” alisema Rais Ruto.
“Ili kufikia hili, tumeongeza pesa za shule zinazotolewa kwa wakati na kuzileta pamoja shule za msingi na sekondari ya chini, chini ya usimamizi mmoja mpana, ili kuimarisha ufadhili na kuboresha masomo.”
Rais Ruto aliyasema hayo alipohutubia mkutano wa kila mwaka wa wakuu wa shule katika Kituo cha Ustawi wa Watoto cha Sheikh Zayed mjini Nyali, kaunti ya Mombasa leo Alhamisi.