Ni afueni kwa familia baada ya mwanasheria Abshir Ahmedsadak Abdi kupatikana akiwa hai baada ya siku kadhaa za shinikizo dhidi ya asasi za usalama kubaini aliko mwanasheria huyo.
Ripoti zinaashiria kuwa Abdi alipatikana akiwa hai katika eneo la Sololo, kaunti ya Marsabit siku 11 baada ya kutoweka kwake.
Abdi alidaiwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana huku maafisa maalum wa usalama wakinyoshewa kidole cha lawama.
Chama cha Wanasheria nchini, LSK na wengineo waliwasilisha kesi mahakamani wakiitaka serikali kubaini hatima ya mwanasheria huyo, ama akiwa hai au amefariki.
“Hata hivyo, tuna mashaka makubwa kwa namna vikosi hivi vya utekaji nyara vinavyofanya kazi. Tumesikia neno hili Kundi Maalum la Utekelezaji wa Operesheni, SOG wakati mhariri wa shirika la habari la Standard alipotekwa nyara, tumesikia neno Kikosi cha Usaidizi, OSU chini ya DCI. Tunasikia maneno ambayo yanaenda kinyume cha muundao wa katiba,” alilalama Rais wa LSK Charles Kanjama akizungumza dakika chache baada ya taarifa za kupatikana kwa mwanasheria Abdi kuchipuza.
“Tunasalia chonjo, tunasalia imara, tunasalia kuwa wasiokata tamaa hadi mwanasheria Abshir na Ayub waletwe mahakamani au tujihakikishie usalama wao na hadi wanaokiuka sheria wawajibishwe.”
Kumekuwa na visa kadhaa vya utekaji nyara katika siku za hivi karibuni nchini, visa ambavyo mashirika ya kutetea haki za binadamu hasa yamevilaani vikali na kutaka wahusika kuwajibishwa.
Serikali imekana madai ya kuhusika kwa asasi zake za usalama katika visa hivyo.