Kenya inaadhimisha miaka 50 ya ushirikiano wa kidiplomasia na Umoja wa Ulaya, EU.
Ili kuadhimisha kipindi hicho cha ushirikiano, Rais William Ruto mapema leo Alhamisi amekutana na wajumbe wa EU pamoja na mabalozi wake katika Ikulu ya Nairobi.
Kwenye kikao hicho, Ruto alielezea ufanisi ulioafikiwa katika kipindi hicho cha nusu karne, ikiwemo katika masuala ya uongozi na demokrasia, sheria ya kimataifa na ushirikiano wa kimkakati.
Amesema kuwa soko la EU hutumia asilimia 21 ya bidhaa kutoka humu nchini, likiwa soko kubwa zaidi kwa bidhaa za kutoka Kenya, na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo wa kiuchumi.
Alipongeza mchango wa EU katika juhudi za kuleta amani nchini Somalia kupitia kwa ujumbe wa majeshi ya Umoja wa Afrika , ikiwemo mchango wa shilingi bilioni 3 kupiga jeki juhudi za majeshi ya Kenya.