Rais Wiliam Ruto, amesema mageuzi ambayo serikali yake imetekeleza katika sekta ya kilimo, yameanza kuzaa matunda, huku wakulima wakinufaika pakubwa.
Akizungumza leo Jumanne kwenye ziara yake ya siku ya tatu katika eneo la Gusii, kiongozi huyo wa taifa alisema sasa wakulima wanapata faida ya kumezewa mate kutokana na bidii yao, baada ya serikali kupunguza bei za mbolea na mbegu, kuwasajili wakulima kidijitali na kuyaondoa makundi ya wakiritimba.
“Wakulima wa kahawa sasa wanapata shilingi 150 kwa kila kilo kutoka shilingi 70 kwa kila kilo hapo awali. Wakulima wa miwa wanapokea malipo yao ndani ya siku saba baada ya kuwasilisha miwa,” alisema Rais Ruto.
Rais alisema serikali itawekeza shilingi bilioni 4.2, kuweka vifaa vipya kwenye viwanda vya Majani Chai kuhakikisha wakulima wanapata bonasi kwa usawa.
Kiongozi huyo wa nchi alizindua ujenzi wa barabara ya Kenyoro SDA-Riana Market-Kerina katika eneo bunge la Bonchari, kaunti ya Kisii.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 22, inatarajiwa kupunguza msongamano, kurahisisha ufikiajo wa soko na kubuni fursa mpya za kibiashara na uwekezaji.