Mwanamuziki nyota wa muziki wa Dancehall kutoka Jamaica, Konshens, anatarajiwa kurejea Nairobi, Kenya, Desemba 18, 2026, kwa tamasha itakayofanyika katika ukumbi wa Sarit Expo Centre.
Tamasha hiyo iliyopatiwa jina la ‘Dancehall Detention with Konshens – The High School Reunion’, imeandaliwa na kampuni za Talent Africa na Homeboyz.
Lengo la hafla hiyo ni kuwapa mashabiki nafasi ya kufurahia upya vibao maarufu vya Dancehall walivyovikulia.
Konshens alitangaza ujio huo kupitia mitandao ya kijamii, akiwakaribisha mashabiki kushiriki katika usiku wa burudani utakaorejesha kumbukumbu za muziki wa zamani.
“Nairobi, mmewekwa kwenye orodha ya wanafunzi watakaoadhibiwa,” aliandika, akidokeza kuwa tamasha hilo litajumuisha midundo maarufu ya miaka ya nyuma.
Tamasha hiyo itafanyika Ijumaa, Desemba 18, 2026, huku tiketi za awali zilizopewa jina la First Bell zikiwa zinauzwa tayari.
Hii itakuwa ziara nyingine ya mwanamuziki huyo nchini Kenya, ambako amejijengea mashabiki wengi na mara kadhaa kueleza mapenzi yake kwa nchi hii.
tamasha ya Nairobi itakuja baada ya nyingine ya mwanamuziki huyo nchini Uganda Desemba 11, 2026, katika uwanja wa Lugogo Cricket Oval jijini Kampala.
Tamasha hiyo ya Uganda imepatiwa jina la Vibe Republic na inasubiriwa kwa hamu huku ikitarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki wa muziki wa Dancehall wanaotaka kushuhudia burudani ya moja kwa moja kutoka kwa mwanamuziki huyo mashuhuri.