Kasita ataka mashabiki kukoma kukosanisha wasanii wa kike

Anasema wasanii wanawake hawapaswi kushinikizwa kuchagua upande katika migogoro ya watu maarufu.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Karole Kasita amewataka mashabiki kuacha kuchochea migogoro isiyo na umuhimu, miongoni mwa wanamuziki wa kike.

Msanii huyo anasema wasanii wanawake hawapaswi kushinikizwa kuchagua upande katika migogoro ya watu maarufu.

Karole alisema waimbaji wanawake wanakabiliwa na matarajio yasiyo ya haki, huku mashabiki wakihoji urafiki na ushirikiano wao kutokana na tofauti zilizopo kati ya wasanii wengine.

Alibainisha kuwa wanamuziki wa kiume hawakabiliwi na ukosoaji kama huo, hata wanaposhirikiana na waimbaji wanawake ambao wana migogoro binafsi.

Kwa mujibu wa Karole, mashabiki hufurahia muziki bila wasiwasi wanaume wanapofanya kazi na waimbaji mbalimbali wa kike, lakini wanawake wanatarajiwa kugombana au kuepuka kushirikiana.

Mwimbaji huyo alisema amekuwa akiepuka migogoro ya watu maarufu katika kipindi chote cha kuwa kwenye tasnia ya muziki na hana nia ya kujihusisha na ushindani huo.

Kauli zake zimekuja baada ya kushirikiana hivi karibuni na Sheebah Karungi, jambo lililozua mjadala kutokana na Karole kuwa shabiki wa Cindy Sanyu, ambaye amekuwa na uhasama wa muda mrefu na Sheebah.

Hata hivyo, Karole amepuuzilia mbali madai kwamba anapaswa kuchagua mmoja wao, akisisitiza kuwa anawapenda na kuwaheshimu wote.

Pia ameeleza utayari wake wa kufanya kazi na Sheebah pamoja na Cindy katika wimbo mmoja, akisema ushirikiano wa wasanii hao watatu unaweza kusisimua tasnia ya muziki nchini Uganda.

Share This Article