Shughuli za uokoaji zilizokuwa zikitekelezwa na asasi mbalimbali za serikali kwenye jengo lililoporomoka Eastleigh, jijini Nairobi, zimekamilishwa rasmi.
Akithibitisha kukamilishwa kwa shughuli hizo, Mrakibu wa eneo la Nairobi Gilbert Osumba, alisema hatua hiyo iliafikiwa baada ya upekuzi uliofanywa katika kila sehemu ya chini ya jengo hilo, kubainisha hakuna waathiriwa zaidi.
Hadi kukamilishwa kwa zoezi hilo la uokoaji, watu wanane walithibitishwa kufariki kutoka kwa mkasa huo, huku watu wanne wakiokolewa wakiwa hai.
Juhudi za uokoaji zilitekelezwa na Vikosi vya Ulinzi (KDF), Huduma ya Taifa ya Polisi, Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), Shirika la Msalaba Mwekundu, na Kitengo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Majanga.
Uchunguzi kuhusu chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo umeanzishwa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya jinai, DCI.