Waathiriwa wa maandamano wamelipwa fidia ya shilingi milioni 96.95 katika awamu ya saba ya mchakato unaoendelea wa kuwalipa wale ambao haki zao zilikiukwa wakati wa maandamano yaliyopita nchini.
Mwenyekiti wa Jopo la Fidia Prof. Makau Mutua anasema kama ilivyofanywa katika awamu sita za awali, malipo yametolewa kwa madai yaliyothibitishwa pekee.
Waathiriwa ambao hawajawasilisha madai yao wana hadi Novemba 14 kufanya hivyo la sivyo wafungiwe nje.
“Tunasisitiza kuwa jopo litakoma kupokea madai mapya ya fidia Novemba 14, 2026. Waathiriwa ambao bado hawajawasilisha madai wanaombwa kufanya hivyo kabla ya kukamilika kwa makataa,” alisema Prof. Mutua kwenye taarifa.
“Jopo linaendelea kupokea madai kupitia njia rasmi mbalimbali na linapiga hatua katika kuyashughulikia na kulipa fidia katika vipengele mbalimbali vya madhara. Tumedhamiria kuhakikisha hakuna anayestahiki kulipwa fidia atafungiwa nje.”
Awamu ya saba inahusisha madai ya waathiriwa ambao ni raia na pia maafisa wa usalama ambao haki zao zilikiukwa wakati wa maandamano.
Jopo linasema madai yote yanayopokelewa yatapigiwa msasa vilivyo ili kuthibitisha uhalali wake kabla ya fidia kulipwa kwa wahusika.