Mwanamuziki wa Kenya Bahati, ametangaza wimbo wake mpya uitwao “Uinuliwe” anaourejelea kuwa wimbo wa shukrani, siku chache tu kabla ya harusi yake.
Katika ujumbe wake wa kutangaza ujio wa wimbo huo Bahati aliandika, “Imekuwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja bila wimbo mpya na tunapotizamia harusi Ijumaa hii, nimehisi niandike barua ya shukrani kwa Mungu”.
Aliendelea kusema kwamba Mungu amekuwa mzuri na mwenye neema ambaye amemruhusu atembee kwa huruma zake, na upendo wake umekuwa wa kujivunia.
“Yote niliyonayo ni kutoka kwa Mungu na Ijumaa hii kweli ni ushuhuda,” aliandika Bahati.
Bahati na mkewe Diana Marua wamekuwa pamoja kwa muda wa miaka 10 na Ijumaa Novemba 6, 2026 ni siku yao ya harusi hafla ambayo imezua gumzo mitandaoni.
Wanandoa hao ambao ni wasanii wa muziki, wamekuwa wakitangaza harusi hiyo ambayo itakuwa na wageni 100 pekee, ambao kila mmoja analipa shilingi milioni moja pesa za Kenya ili kuhudhuria.
Mashabiki wengi wa wawili hao wamekuwa wakilalama mitandaoni kwamba kiingilio hicho ni cha juu sana na wengi hawataweza kumudu.
Inasubiriwa kuona jinsi hafla hiyo itakuwa, ikikumbukwa kwamba imegharimu wahudhuriaji hela nyingi.
Tazama video ya wimbo huo mpya hapa;